WAOMBOLEZAJI WAMWAGA CHAKULA MSIBANI HUKO KILEMA MOSHI, TANZANIA WADAI MAREHEMU HAKUWA AKIPEWA CHAKULA ALIPOKUWA HAI






 WAOMBOLEZAJI WAMWAGA CHAKULA MSIBANI HUKO KILEMA MOSHI, TANZANIA WADAI MAREHEMU HAKUWA AKIPEWA CHAKULA ALIPOKUWA HAI


Waendesha bodaboda wa kituo cha Kisangiro kata ya Kilema Kaskazini wilayani Moshi Mkoa wa Kilimanjaro wamevamia msiba wa Lenard Abel (20) na kumwaga chakula na pombe kwa madai kuwa ndugu na majirani wa marehemu wakimtelekeza hawakumsaidia chochote alipokuwa hai hata chakula tu walishindwa kumpa hali iliyolazimu bodaboda hao kupeana zamu za kumpelekea chakula.


Walifika katika msiba huo saa 9 alasiri jana Jumatatu Mei 3, 2021 baada ya mazishi wakati mwenyekiti wa ukoo akitoa ratiba ya chakula na kumwaga chakula hicho kitendo kilichozua tafrani na waombolezaji kulazimika kutimua mbio.


Shuhuda wa tukio hilo, Lucy Lyimo amesema kundi hilo la vijana lilifika msibani na kuvamia jikoni na kuanza kumwaga chakula na pombe aina ya mbege sambamba na kuvunja viti.


“Wakati mwenyekiti wa ukoo akitoa ratiba ya chakula kulitokea kundi la vijana zaidi ya ishirini wakipiga ukunga na kusema huyu marehemu kipindi akiwa hai alikuwa hapewi chakula iweje leo amekufa chakula kipo na pombe, " amesema Lucy akibainisha wakati wakisema hayo walikuwa wakielekea ilipohifadhiwa pombe na chakula


Amesema walipomwaga chakula na pombe waliwasha mishumaa na kuelekea makaburi yalikofanyika mazishi.


Mwenyekiti wa kijiji cha Kyou, Paul Lyimo amesema wakati vijana wakifanya vurugu za kumwaga chakula na vinywaji Padri wa Parokia ya Kilema aliyeendesha ibada ya mazishi aliwafuata kuwaomba wasifanye vurugu ila hawakusikia.


"Padri aliwapigia hadi magoti kuwaomba wasifanye hivyo lakini waliendelea kumwaga chakula huku wakipiga ukunga na baada ya hapo walienda kuwasha mishumaa kwenye kaburi na kutawanyika," amesema.


_____

NOTE: Kuna haja gani ya kuonesha unafiki wa kufanya mazishi ya kifahari kwa mwendazake marehemu ili hali hatukumjali alipokuwa hai? Kuna faida gani kutumia mamilioni ya shilingi kuonesha ufahari msibani huku baada ya msiba tukizitelekeza familia watoto na hata mjane wa mwendazake?


Ni unafiki na kufuru kunamjali sana marehemu kuliko mgonjwa au mtu alie hai ambaye ulikuwa na nafasi ya kumsaidia lakini ukangoja afe ili jamii ikuone wewe una pesa siku ya mazishi.


Ni unafiki na kufuru kunatumia gharama kubwa za mazishi na tunajitolea sana lakini hatujitolei kuokoa maisha ya mgonjwa. 


Ni unafiki kujifanya kuwa upo bize na mambo yako na huna muda wa kwenda kutizama mgonjwa lakini akifa tunapata muda wa kwenda kukesha msibani.


Wengine hawajahi kupata kabisa zawadi za maua lakini wakifariki yatakuja mengi sana juu ya kaburi lake. This is none sense.


Tutapamba kaburi kwa marumaru hata kama nyumba ya marehemu haikuwai kuwekewa marumaru. Je tulimuacha aishi kwa ufikara ili maiti yake ioze kifahari?


Tumekuwa wanafiki kupitiliza wakati mwingine ukifuatilia ripoti ya daktari unaambiwa marehemu alidhoofu kutokana na lishe duni na msongo wa mawazo baada ya kutelekezwa na ndugu, watoto na hata marafiki. Wanafiki hawahawa siku ya mazishi utaona wakiingia na pikapu iliyosheheni vyakula na jeneza la kifahari ambalo nusu ya gharama yake ingetosha kuokoa maisha ya mwendazake kwa kupata tiba na lishe bora....


Lazima tujue thamani ya Maisha kuliko Kifo tuache UNAFIKI

Comments

Popular posts from this blog

NI SABABU ZIPI ZINAZOFANYA MZUNGUMZAJI WA LUGHA KUFANYA MAKOSA YA KISARUFI NA KIMATAMSHI NA KIMANTIKI KATIKA LUGHA?

Methali, Vitendawili, nahau, misemo,

NADHARIA ZINAZOELEZEA CHIMBUKO LA FASIHI SIMULIZI/MASIMULIZI