NADHARIA ZINAZOELEZEA CHIMBUKO LA FASIHI SIMULIZI/MASIMULIZI
NADHARIA
ZINAZOELEZEA CHIMBUKO LA FASIHI SIMULIZI/MASIMULIZI
Kazi hii tumeigawa katika sehemu tatu, ambazo ni, Utangulizi, katika
sehemu hii tutatoa fasili ya nadharia na fasili ya ngano kwa mujibu wa
wataalamu mbalimbali. Sehemu ya pili itakuwa ni kiini cha swali ambapo
tutajikita kuzielezea nadharia mbalimbali zinazozungumzia asili ya fasihi
simulizi/masimulizi kwa mujibu wa Okpewho (1992), Miruka (1994/1999) na
Finnegan (1970). Na sehemu ya mwisho ni hitimisho.
Tukianza na fasili ya Nadharia, Massamba
(2009:63) anasema, nadharia ni taratibu kanuni na misingi ambayo imejengwa
katika muundo wa kimawazo kwa madhumuni ya kutumiwa kama kielelezo cha kuelezea
jambo. Sarantakos (1997: 9) amefasili nadharia kama jambo linalofanywa na
kuthibitishwa kwa utaratibu maalum kwa njia ya utafiti kwa ajili ya kuelezea
jambo fulani katika jamii. Martin E. Amini (2005:10) anasema nadharia ni jumla
ya mambo yote ambayo mtafiti amekusudia kuelezea, kuchambua, kuelewa au hata
kutabiri jambo fulani kwa utaratibu maalum.
Hivyo basi, nadharia huchukuliwa kama
dira au muongozo wa kumuongoza mtafiti/mchambuzi ili kulielezea vema jambo
fulani kwa mtazamo unaotarajiwa kuwa imara zaidi kuliko mtazamo mwingine. Hivyo
tunaweza kujumuisha kuwa nadharia ya fasihi simulizi ni chombo kinachotoa
mwongozo kuhusu mwelekeo wa jamii fulani.
Maana ya ngano
Senkoro (2011:53) anasema,
ngano ni utanzu wa kifasihi simulizi ambao ulipitishwa toka kizazi
kimoja hadi kingine kwa njia ya mdomo. King’ei (2005:65)
anasema ngano kuwa ni hadithi fupi na
zenye masimulizi yasiyo
ya kishairi. Kwa upande wake,Wamitila, K.W. (2003:165) anasema
ngano ni hadithi ya kale ambayo ni moja kati ya tanzu maarufu za fasili simulizi.
Ni moja kati ya vipera au vitanzu vya hadithi au simulizi. Ngano nyingi huwa na
mwanzo wa hapo zamani za kale.
Kwa fasili yetu, tunaweza kusema
kuwa, ngano ni utanzu wa hadithi fupi fupi ambazo huelezea/kusimulia matukio
mbalimbali yanayoleta mafunzo katika jamii husika na kurithishwa kutoka kizazi
kimoja hadi kingine.
Baada ya kuangalia fasili mbalimbali
za nadharia na ngano, sehemu inayofuata ni kuzielezea nadharia mbalimbali
zinazozungumzia asili ya fasihi simulizi/masimulizi kwa mujibu wa Okpewho
(1992), Miruka (1994/1999) na Finnegan (1970). Tukianza na Okpewho (1992)
ameanisha aina sita za nadharia zinazoelezea asili ya fasihi
simulizi/masimulizi ambazo ni, nadharia ya mabadiliko, nadharia ya msambao,
nadharia ya uamilifu, nadharia ya urasimi, nadharia ya Saikochanganuzi na
mwisho ni nadharia ya Umuundo. Kwa upande wake, Miruka (1994) ameanisha aina
tano za nadharia ambazo ni, nadharia ya Mabadiliko, nadharia ya msambao,
nadharia ya urasimi, nadharia ya uamilifu na nadharia ya umuundo, wakati
Finnegan (1970) ameanisha aina tatu za nadharia ambazo ni nadharia ya
Mabadiliko, nadharia ya msambao na nadharia ya Umuundo.
Tukiangalia uanishaji wa nadharia
hizo za wataalamu hapo juu, tunaona kuwa, wataalamu hao wanatofautiana katika
idadi ya nadharia hizo, lakini kimsingi wataalamu wote wanakubaliana kuhusu
nadharia fulani fulani, mathalani, wote wanakubaliana uwepo wa nadharia ya
mabadiliko, nadharia ya msambao na nadharia ya umuundo. Lakini Okpewho na
Miruka wanakubaliana juu ya uwepo wa nadharia ya mabadiliko, nadharia ya
msambao na nadharia ya umuundo, nadharia ya urasimi na nadharia ya uamilifu.
Okpewho anainisha aina nyingine ya nadharia ya Saikochanganuzi ambayo
haijitokezi kwa hao wataalamu wengine. Hivyo katika uwasilishaji wetu,
tutazigawa nadharia hizo katika aina sita kama ifuatavyo:
Nadharia ya wanamabadiliko, nadharia hii
iliasisiwa na Charles Darwin ambaye alikuwa mwana bailojia karne ya 19,
alifanya utafiti kuhusu mabadiliko ya viumbe ambao waliishi miaka mamilioni
iliyopita. Katika utafiti wake aligundua kuwa viumbe walioendelea kuishi
imewezekana tu kwa sababu ya kumudu mapambano dhidi ya uhaba wa vyakula, hivyo
Darwin aliita jambo hili kama “Uhai kwa wanaofaa”. Pia aligundua viumbe
walioendelea kuishi kwa sababu ya maumbo yao na mazingira yaliyosababisha wao
kuwepo.
Mawazo ya utafiti wa Darwin yalishadadiwa
na wanazuoni mbalimbali waliokuwa wanachunguza utamaduni wa binadamu, katika
utafiti wao walikusanya simulizi kutoka jamii mbalimbali za Afrika, Asia na
Amerika ambapo baada ya kukusanya simulizi hizo waligundua zilikuwa na ufanano
wa kimaudhui. Wanamabadiliko wanaamini kuwa ngano/masimulizi tuliyonayo leo
yana asili moja isipokuwa zimekuwa zikibadilika kutokana na mabadiliko ya
wakati. Zaidi ya haya wanamabadiliko wanaamini kuwa viumbe wote tumetokea
kwenye asili moja hivyo tuna uwezo wa akili sawa na maendeleo tutakuwa sawa.
Ubora wa nadharia hii, nadharia hii ndiyo
msingi wa nadharia nyingine zilizofuata kama nadharia ya msambao, urasimi na
uamilifu. Vilevile imesaidia kuelezea asili ya ngano/masimulizi hasa ngano
zinazofanana kimaudhui, na mwisho nadharia imesaidia kuonesha kuwa ngano zina
asili moja isipokuwa zinabadilika kutokana na mabadiliko ya wakati na
mazingira.
Mapungufu ya nadharia hii, wanamabadiliko
waliamini kila kilichokusanywa katika fasihi simulizi kilihesabika kama masalia
ya zamani/mabaki ya fasihi zilizotangulia, kwa maana kwamba kila kitu
kilichosalia kitakuwa na dosari hakiwezi kuwa kitu halisi. Wanamabadiliko pia
wameangalia tu upande wa maudhui na kuacha kipengele cha fani kama vile muundo
na mitindo ya fani husika. Mwisho, pamoja na ufanano wa huo wa kimaudhui kuwa
ngano zina asili moja lakini kuna tofauti kubwa hasa katika utendaji wa fanani
hivyo fanani hutofautiana.
Nafasi ya nadharia hii katika ngano
za Kiswahili, nadharia hii inahusiana na ngano za Kiswahili katika sanaa za jadi
ambayo ni elimu inayohusu asili ya binadamu pamoja na umuhimu wake ambao
ilihusishwa na usimulizi wa ngano ambayo ilitokana na jamii husika katika
shughuli mbalimbali za jamii kama vile jando na unyago, miviga, vyanzo vya
vyakula, sherehe, matambiko kwa kutaja kwa uchache.
Nadharia ya msambao, nadharia hii
imeasisiwa na wataalamu kama Jacob na Wilhem Grimm, baadaye mawazo yao
yaliendelezwa na Maxmuller na Mmarekani Stere Thomson. Pamoja na kwamba
kulikuwa na tofauti ndogondogo lakini wataalamu wa nadharia hii wanamwelekeo
mmoja ambao wanaamini kuwa chimbuko la fasihi simulizi ni moja lakini kutokana
na maingiliano ya kijamii ndiyo yaliyosababisha kusambaa kwa hii ngano hasa
kutoka katika jamii zilizostaarabika (Ulaya) kuja katika jamii zisizostaarabika
(Afrika).
Okpewho anasema, wanamsambao
walijishughulisha na kuhusianisha ngano za jamii mbalimbali na kugundua kuwa
ngano zina ufanano unaokaribiana sana. Uhusiano huu unahusishwa na kipindi cha
kihistoria ambacho kulikuwa na mawasiliano baina ya jamii moja hadi nyingine.
Katika utafiti wao wanamsambao wamegawanywa katika shule mbili, kwanza ni kundi
la shule ya India, kundi hili lilianzishwa na Jacob na Wilhelm ambapo
walikusanya hadithi mbalimbali huko ujerumani na kwingineko barani Ulaya na
kugundua kuwa ngano hizo zilikuwa na uhusiano na kuhitimisha kuwa ngano za
Ulaya kama zilivyo lugha za Ulaya zimeonekana na rangi ya nasaba bora iliyopata
kuishi huko kati ya kaskazini na Asia, rangi ya nasaba bora si rangi ya ngozi
bali ni familia ya lugha ambayo lugha zote za Ulaya zinahusishwa nayo. Hivyo
aligundua kuwa ngano zilikuwa zinasambaa na makundi ya wahamiaji. Wao waliona
chimbuko la ngano ni huko India na zikafika huko Magharibi kwa njia ya msambao.
Kundi la pili ni kundi la shule ya
Kifini, shule hii ilianzishwa na Eliasi Lonnrot ambaye mwaka 1825 alianza
kukusanya ngano za mashujaa katika nchi ya Finland, kupitia maudhui
yanayohusiana na kuziweka katika kundi moja.
Ubora wa nadharia hii, wanamsambao
waliipa hadhi fasihi simulizi kwa kuchunguza muktadha kwa undani, vilevile,
nadharia hii ilionekana kuwa ni ya kisayansi zaidi, hivyo inaweza kuchunguzika
tofauti na wanamabadiliko kwani akili ya mtu haiwezi kuchunguzika.
Upungufu wa wa nadharia hii, kufikiria
kuwa ngano zimeenea toka kundi moja la watu hadi kundi jingine, inaonesha kuwa
jamii ya Kiafrika haikuwa na ngano. Nadharia hii inaona kuwa Afrika haikuwa na
ngano kwani ngano zilitoka katika jamii zilizostaarabika (Ulaya) jambo ambalo
si kweli kwani hata kabla ya ujio wa wakoloni Waafrika walikuwa na ngano zao.
Vilevile, licha ya kuipa fasihi simulizi upekee katika kipengele cha muktadha
lakini hawakuchunguza kwa undani vipengele vya kisanaa vya fasihi simulizi,
mfano hawakuangalia vipengele muhimu vya fasihi simulizi ya Kiafrika hususani
sanaa ya jadi kama vile, miviga, jando na unyago, matambiko, n.k.
Nafasi ya nadharia hii katika
ngano za Kiswahili, ukiangalia kwa jicho la ndani nadharia hii inasaidia
kutambua kuwa mfanano wa ngano katika jamii nyingi za kiafrika ulitokana na
maingiliano ya shughuli za kijamii kama vile, biashara, kilimo,ufugaji,
uwindaji na kazi mbalimbali za jamii.
Nadharia ya umuundo, nadharia hii
iliasisiwa na Claude Levis Strauses, alidai kuwa utamaduni unajumuisha vitu
mbalimbali vinavyofanana, alichunguza visasili na kusema kuwa visasili hivyo
vinatumika katika kuelezea na kutatua matatizo katika jamii. Hadithi hizo
zilikuwa zinaelezea falsafa ya jamii husika, alidai kuwa visasili hivyo
vilisaidia jamii katika kuyaelewa na kutatua matatizo ambayo yalileta mtanziko
katika maisha ya binadamu, matatizo hayo ni kama vile, uhai na kifo.
Strauses, alidai kuwa muhusika wa
ngano anajengwa katika kupambana na tatiziko ambalo anashindwa kulipatia
majibu. Dominique Zahen aliongeza kuwa ngano zinahusu uhai na kifo na
ziishie kwa kuona kuwa uhai na kifo vimetoka kwa mungu (mfano: ngano
inayoelezea namna kifo kilivyoingia duniani) (rejea Miruka 1994:138)
Ngano zinatakiwa kutazamwa kama mfumo
wenye kanuni zake ambazo kila msanii anatakiwa kuelewa pia aelewe mfumo
unavyoweza kutumiwa katika mawasiliano na hata kimuundo. Mfano katika ngano
lazima kuangalia matumizi ya lugha na kaida zinazotawala utunzi huo.
Ubora wa nadharia hii, nadharia
hii inasisitiza kuwepo kwa kanuni/kaida maalumu za kiutambaji, kiutunzi na
matumizi ya lugha. Hapa wanaona kuwa ngano zisichukuliwe kama kitu pekepeke
bali ni utanzu unaoongozwa na kaida maalumu katika uumbaji, kiutambaji na
matumizi ya lugha. Hivyo kutakuwa na sifa zinazofanana katika ngano zote.
Vilevile, inasaidia kujua chimbuko la ngano katika jamii fulani.
Udhaifu wa nadharia hii, kwanza kwa
kutumia nadharia hii hatuwezi kupata kanuni rasmi ya kiutambaji, kiutunzi na
matumizi ya lugha toka jamii moja hadi nyingine. Hii ni kutokana na ukweli
kwamba kila jamii ina namna yake ya kuwasilisha ngano zao, kuziumba ngano zao
na matumizi ya tofauti ya lugha. Mfano; maumbo ya ngano yanatofautiana toka
jamii moja hadi nyingine, mfano, muingiliano wa tanzu moja katika nyingine,
utambaji pia hutofautiana, mfano watambaji na tabaka tawala na watambaji na
tabaka duni. Hata wahusika wa ngano pia hutofautina mhusika anaweza kuwa mtu
duni kwenda bora au mtu bora kuwa mtu duni. Nadharia hii pia inatalia mkazo
muundo kuliko dhima ya ngano katika jamii.
Nafasi ya nadharia hii katika
ngano za Kiswahili, nadhairia inasaidia wanafasihi kutambua/kuelewa ngano kama
utanzu wa fasihi una muundo wake rasmi katika uumbaji, kiutambaji na matumizi
ya lugha kiulemwengu lakini muundo huo si wa kimajumui kwa maana huweza
kutofautiana kutoka jamii moja hadi nyingine.
Nadharia ya urasimi, nadharia hii
iliasisiwa na mwanazuoni wa Kinesi Vladimir Propp (1928,1968) katika chake
cha “The Morphology of the folktale.” Nadharia hii ilizuka ili
kupinga mawazo ya wanamsambao hususani katika ugawaji wa ngano bila kuchunguza
kwa umakini sifa ya kila kundi. Propp anaamini kuwa ili kuchunguza asili ya
ngano ni vema kuanza kuchunguza aina za ngano kwa kuangalia maumbo ya ngano.
Hivyo mtazamo huu unaangalia asili ya ngano kwa kuchunguza maumbo ya ngano
husika.
Ubora wa nadhairia hii, nadharia
hii inasaidia kujua aina za ngano kutokana na dhima zake, mfano ngano za
urafiki, miadi, ukatili, ugunduzi na mwisho wa urafiki, (Alan Dunde’s)
Udhaifu wa nadharia, nadharia hii
inaonekana kutomzingatia mtambaji ambaye ni sehemu ya ngano yenyewe ambaye
anaweza kubadilisha umbo la ngano kadri ya utendaji wake.
Nafasi ya nadharia hii katika ngano
za Kiswahili, nadharia hii inatusaidia kuziweka ngano katika makundi kutokana
na kazi zake. Mfano tunapata ngano zinazohusu wahusika wajanja mfano sungura na
wahusika wasiowaelevu/wajinga mfano fisi.
Nadharia ya saiko-changanuzi, muasisi wa
Nadharia hii ni Sigmund Freud raia wa Australia, mtaalamu huyu alikuwa tabibu
wa magonjwa ya akili, alifanya uchunguzi wa nafsia, alichunguza hasa sehemu ya
nafsi iliyofichika yaani sehemu ya ung’amuzi bwete ili kujua asili ya tatizo la
mgonjwa husika, alieleza kuwa ung’amuzi bwete ni sehemu ya akili ya binadamu
ambayo huhodhi fikra, mawazo, hofu na mitazamo hasi ambayo haiwezi kukubalika
na jamii. Hofu na mawazo hayo hujitokeza kwa ndoto. Pia ung’amuzi bwete
huhusisha matukio yaliyotendeka zamani lakini mgonjwa huyaingiza katika
maongezi yake kama yanatendeka muda huo. Kutokana na utafiti wake aligundua
kwamba ndoto zote husheheni ukweli kuhusu maisha ya mgonjwa.
Freud anaifananisha kazi ya fasihi na
ndoto kwa kuwa visasili huwa ni hadithi za kubuni basi ubunifu huo unashabihi
ndoto kwani wahusika wake na maudhui yake kwa ujumla huwa katika
ulimwengu wa kufikirika ambao ni kama ndoto katika ulimwengu halisi sawa sawa
na mgonjwa wa akili anayeumba ulimwengu wake.
Freud alisisitiza mambo yote katika
akili ya binadamu yanatawaliwa na ngono (libido). Mawazo yake yaliungwa mkono
na mwanafunzi wake Carl Gustav Jung ambaye pia alifanya kazi pamoja na Freud
katika kuwatibu wagonjwa wa akili kwa kutafsiri ndoto ingawa Gustav
alitofautiana na Freud kwa msimamo wake kuwa akili ya binadamu inatawaliwa na
ngono.
Carl Gustav Jung alifanya utafiti na
kuunda dhana ya kikale ambayo ni mtiririko au picha kongwe inayojitokeza mara
kwa mara katika tajriba anayopitia mwanadamu , alisema kuna sehemu ndani ya
akili isiyokuwa na fahamu ya mtu mwenyewe lakini ina athira kubwa juu ya mawazo
na matendo yake. Alitofautisha sehemu hiyo kama, sehemu ya kwanza ni sehemu
binafsi inayofunza maarifa yaliyokusanywa na kila mtu katika maisha yake na
sehemu ya pili ni sehemu ya kijamii inayofunza maarifa ya kibinadamu
yaliyokusanywa na watu katika historia yao na kuendelezwa kwa karne nyingi.
Anasema sehemu hii husika na matambiko muhimu ambayo mtu anapitia kama sherehe
za kumpa mtu jina, sherehe za kuingia jandoni na unyagoni, sherehe zinazoigizwa
wakati wa ndoa na hatimaye sherehe zinazohusu maziko ambazo sherehe zote hii
ndizo huibua ngano.
Gustav alifafanua kwa undani masuala
ya ngano katika tamaduni mbalimbali za dunia. Hivyo Freud na Gustav wanasema
masimulizi ni kama ndoto au mvurugiko wa akili kwani picha, taswira na maudhui
vyote ni vya kubuni havitoki katika ulimwengu halisi.
Ubora wa Nadharia hii, Nadharia hii
inaonesha utofauti wa msimulizi mmoja hadi mwingine hutokana na historia ya mtu
binafsi na uwezo wake binafsi hata kama kisa kitakachosimuliwa ni kimoja, hii
imedhihirishwa kwa wagonjwa waliokuwa wanasimulia mambo yao kwa utofauti
kutokana na historia zao. Lakini pia imesaidia kutuonesha chimbuko la ngano kwa
miktadha tofauti tofauti kama sherehe za jando na unyago, sherehe za kutoa
jina, n.k.
Upungufu wa Nadharia hii, Nadharia
hii imesisitiza zaidi masuala ya hisia za kingono katika ubunifu wa masimulizi
kitu ambacho hakina ushahidi wa kutosha kwani siyo kila hadithi inatarajia
kujiridhisha kutoka hali ya ngono iliyofifizwa katika ung’amuzi bwete kama
anavyosema Freud.
Nadharia ya kiuamilifu, Nadharia hii
iliasisiwa karne ya 20 na Poland Bronislav Malinowsk. Uamilifu uliibuka kama
njia yal kuyatazama maisha na utamaduni wa jamii, kwa kuchunguza dhima za
vipengele vya kijamii pamoja na njia ambazo kwazo dhima hizi zinahakikisha
uwepo wa jamii. Malinowsk alifanya utafiti Australia na kugundua kuwa ngano ni
kumbukumbu za kweli za mila na desturi za jamii zilizopita, unyago, jando,
mazishi, harusi, tohara, matambiko, kusalia miungu, n.k.
Ubora wa Nadharia hii, Nadharia hii
imesaidia kuondoa mawazo kuwa chimbuko la fasihi mbalimbali zikiwemo ngano ni
mahali fulani bali ni kila jamii imekuwa na simulizi ambazo zinasawiri tajriba
(uzoefu) wao wa kila siku katika Nyanja mbalimbali kama vile, kiuchumi,
kisiasa, kiutamaduni na kijamii. Vilevile Nadharia hii, inatusaidia kujielewa
na kuzielewa jamii zetu vizuri, kwa kuyaelewa mazingira ya mila na desturi zetu
katika jimii.
Nafasi ya Nadharia hii katika
ngano za Kiswahili, inatusaidia kujua tamaduni zetu katika somo la ngano, pia
inatusaidia kujua kuwa kila jamii ilikuwa na tamaduni zao zenye kuwaongoza
katika maisha yao ya kila siku kama vile, jando na unyago, harusi, matambiko,
mazishi, miviga, kusalia miungu kuwa ndiyo chimbuko la ngano.
Hitimisho, kila nadharia
tuliyoiangalia ina umuhimu wake katika kujifunza chimbuko la ngano, hivyo ni
muhimu kila mwanataaluma wa ngano kuzisoma na kuzielewa nadharia zote
zinazozungumzia chimbuko la ngano kwa sababu kila nadharia ina misingi yake
ambayo kwa namna moja ama nyingine inatusaidia kujua na kuelewa chimbuko la
ngano, Nadharia hizi ni muhimu pia kujifunza kwa sababu kuanzishwa kwa nadharia
inategemea na upungufu unaojitokeza katika nadharia nyingine. Kwa ujumla licha
ya mtenguo wa nadharia moja dhidi ya nyingine tunaona kuwa Nadharia hizi
zinakamilisha, Nadharia moja inakamilisha Nadharia nyingine. Kwa maana hiyo,
hatuwezi kujua au kuthibitisha chimbuka la ngano kwa kutumia nadharia moja.
MAREJEO
Finnegan, R. (1976) Oral
Literature in Africa. Oxford University Press. Nairobi.
Kingei, K na Kisovi, C (2005), Msingi
wa Fasihi simulizi. Nairobi: Kenya Literature
Bureau.
Martin E.Amin (2005),Social
Science Researc Conception,Methodology and
Analysis.Makerere University
Massamba (2009:63) Kamusi ya isimu na
lugha, Falsafa ya Lugha. Dar es salaam.TUKI.
Mhando,J. na Balisidya, N. (1976) Fasihi , Tanzania
Publishing House, Dar es salaam.
Miruka, O.S. (1994) Encounter
with Oral Literature, East African Educational
Publisher.Nairobi. Kenya.
Muhando, P & Balisidya, N
(1976) Fasihi na Sanaa za Maonyesho. Tanzania
Publishing
House(TPH)
Dar es Salaam.
Mulokozi, M.M. (1989:5) “Tanzu
za Fasihi Simulizi” Katika MULIKA Na. 21, D.SM. TUKI
Nkwera, F.V. (xx) Tamrini za
Fasihi Simulizi: Sekondari na Vyuo, Dar es Salaam: Business
Printers
Limited
Okpewho, I. (1992) African
Oral Literature. Backgrounds, Character, and Continuity.
Indiana University Press: USA.
Sarantakos. S.(1997), Social
Research. (2nd Edition) Palgrave Publisher Ltd
(Formerly
Macmillan Press Ltd)
Senkoro, F.E.M.K (2011) Fasihi. KAUTITU Limited.
Dar es salaam.
Wamitila. K.W. (2003) Kamusi
ya Fasihi Istilahi na Nadharia. Focus Books.Nairobi.
Kazi hii imeandaliwa kwa pamoja na wanafunzi wa mwaka wa kwanza UDSM:
M.A. Kiswahili.
Comments
Post a Comment